MIAKA 23 BAADAYE, SABABU YA KIFO CHA MWALIMU JULIUS K. NYERERE YAFICHULIWA.
Habari za kuumwa kwa Mwl (77) zilianza kuandikwa na magazeti nchini toka mwezi wa Septemba 1998 ingawa ilikuwa haielezwi alichokuwa anaumwa.
Kutokana na kuumwa huko Mwl ambaye pia ni mwenyekiti wa Taasisi ya mwalimu Nyerere na Tume ya ushirikiano ya nchi za kusini, alilazimika kuahirisha baadhi ya shughuli muhimu ,ikiwamo ya kusimamia usuluhishi wa mgogoro wa Burundi, akiwa ndiye mpatanishi wa kimataifa wa mgogoro huo.

Kabla ya kupatiwa matibabu nje ya nchi ,Mwl alikuwa kijijini kwake Butiama ,Mkoani Mara ambako wakati fulani daktari wake ,Profesa David mwakyusa alilazimika kumfuata hukohuko.
Gazeti moja linalochapishwa Kenya mara moja kwa wiki katika Toleo lake mwanzoni mwa Septemba 1999 liliandika kwamba mwanzoni mwa mwaka 1999, daktari mmoja wa kutoka ujerumani alimfanyia mwalimu uchunguzi wa ugonjwa wa kansa ya damu ) leukemia) ingawa hazikuwepo taarifa zaidi kuhusu majibu ya uchunguzi huo.
Kwa mujibu wa gazeti hilo, wasiwasi kuhusu afya ya Mwl ulianza wakati aliposhindwa kuhudhuria maombelezo ya msiba wa mama wa aliyewahi kuwa waziri mkuu. Joseph Warioba, umbali mfupi kutoka nyumbani kwa Mwl zaidi ya miezi miwili iliyopita.
Habari za Mwl kwenda nje ya nchi kwa ajili ya kupata matibabu zilithibitishwa kwa mara ya kwanza na msadizi wake, Charles sanga ,agosti 30, mwaka 1999 alipozungumza na gazeti la MTANZANIA kwa simu kutoka nyumbani kwa Mwl ,Msasani Dar es salaam Siku Mwl Nyerere alipowasili Dar es salaam kutoka Butiama.
Siku moja baadae ,yaani Agosti 31, Mwl Nyerere aliondoka nchini kwenda uingereza kwa ajili ya matibabu akiwa ameongozana na mkewe Maria Nyerere daktari wake Profesa David mwakyusa na msadizi wake Sanga.
Mjini London, Mwl na ujumbe wake ,walikuwa wakiishi katika nyumba binafsi karibu na ubalozi wa Tanzania ,uingereza, eneo la Green park .
Ijumaa usiku, Septemba 24: hali ya wasiwasi ililizingira jiji la Dar es salaam baada ya Uvumi kwamba Mwl Nyerere alikuwa amefariki dunia.
Septemba 25: Habari zilizopatikana kutoka London zilisema Mwl Nyerere alikuwa bado yuko hai, ingawa hali yake ilikuwa mbaya zaidi na alikuwa amelazwa katika hospitali ya St, Thomas ,eneo la Waterloo, London.
Kwa mujibu wa habari hizo ,hali ya Mwl Nyerere ilibadilika ghafla jumanne Septemba 21, na hivyo ikalazimika alazwe hospitalini.
Watoto wawili wa kike wa mwalimu ,Anna na Rosemary waliondoka kwenda London kutokana na hali ya baba yao kuwa mbaya.
Mama maria Nyerere naye alilazimika kufanyiwa operesheni ya macho baada ya matatizo ya shinikizo la damu kuathiri macho yake.
Kabla ya hali yake kuwa mbaya ,Mwl alikutana na wageni Wengi ,akiwamo Katibu mkuu wa umoja wa nchi za afrika ( OAU) salim Ahmed salim ,mbunge wa karagwe na rafiki yake wa miaka mingi ,George kahama, na hata kuendesha shughuli za ofisi yake ya ushirikiano wa nchi za kusini ( south commission).
Spika wa bunge la muungano ,pius msekwa alimwona Mwl Nyerere baada ya hali yake kuwa mbaya ,msekwa alipitia London akitokea kwenye mkutano wa kamati ya mabunge ya jumuiya ya madola uliofanyika Trinidad na Tobago.
Habari zilisemwa kabla ya hali yake kubadilika ghafla
Septemba 21, Mwl Nyerere alikuwa akiwaambia wageni waliomtembelea katika nyumba alikokuwa akikaa kuwa alikuwa anakusudia kukutana na waandishi wa habari baada ya kurejea nyumbani.
" alikuwa akipiga gumzo la kila aina ,kama kawaida yake kuendesha utani na kuchekesha sana, alisema kwamba alikuwa anakusudia Kukutana na waandishi wa habari baada ya kurejea na kuwaonyesha kuwa hali yake ni nzuri sana" alisema mmoja wa watu ambao alizungumza na gazeti la Mtanzania.
Septemba 26: Mwl aliwekwa kwenye chumba maalum cha wagonjwa wanaohitaji kuangaliwa wakati wote katika hospitali ya st. Thomas ,baada ya hali yake kuwa mbaya zaidi.
Ilielezwa kuwa Mwl Nyerere alihitaji kubadilishwa damu ,lakini madaktari walikuwa wanashindwa kufanya hivyo kwa sababu ya hali yake kuwa mbaya na alikuwa amewekwa kwenye mashine maalum ya msaada kwa ajili ya kumuongezea hewa ya oksijeni.
Uchunguzi zaidi uliofanywa ulionesha kwamba pamoja na leukemia ,alikuwa ana malaria na uchunguzi kwenye mkojo wake ulionyesha ya kuwa alikuwa na maambukizi ' infection'
Septemba 27: Rais Benjamin mkapa ,akizungumza na waandishi wa habari Ikulu Dar es salaam ,baada ya kurejea kutoka katika ziara ya Marekani aliwasihi watanzania kumwombea Mwl Nyerere kwa sala na dua aweze kupona.
" Ninawaomba watanzania wote kila mmoja katika imani yake ,watoe sala na dua za kumtakia Mwl Nyerere arudie afya njema ,apate nguvu za kurejea kwa wananchi wake", alisema mkapa.
Mkapa ambaye alipitia London Septemba 26, kumwona Mwl Nyerere lakini hakuweza kuzungumza nae kutokana na hali yake kuwa mbaya ,alithibitisha kwamba Mwl aligundulika ana kansa ya damu( chronic lymphocytic leukemia), tangu agosti mwaka 1998, ugonjwa ambao huwapata watu wenye umri mkubwa, alisema mkapa.
Alisema wakati huo wataalamu hawakuona dalili zozote za zilizoonyesha haja ya tiba kwa sababu ugonjwa huo hauhitaji matibabu hadi unapofikia hatua fulani. Kinachohitajika ni uchunguzi wa mara kwa mara, alisema Mkapa.
Rais alisema kutokana na hali hiyo na ushauri wa wataalamu ,Mwl alifanyiwa tena ukaguzi wa damu yake Novemba mwaka 1998, na Mei mwaka huu.
" kansa ya damu huwapata watu wenye umri mkubwa na moja ya athari zake ni kupunguza kinga ya mwili kuhimili maradhi .hali hii ilisababisha baba wa taifa kupatikana na ugonjwa wa mkanda wa jeshi ( shingles) Julai mwaka huu" alisema mkapa.
Alisema kwamba tangu mwanzo serikali imechukua hatua zinazohitajika kuhakikisha Mwl anapata matibabu mazuri na yanayohitajika.
Septemba 27: zilipatikana habari kwamba Rais Mstaafu wa Zanzibar ,Idris Abdulwakil ambaye umri wake ulikuwa katikati ya miaka ya 70 kwa mwaka ule wa 1999, naye alikuwa mgonjwa na angesafirishwa kwa dharura kwenda katika hospitali ya St. Thomas aliyokuwa amelazwa Mwl Nyerere kwa ajili ya matibabu ya moyo, Abdulwakil alikuwa Rais wa Zanzibar kuanzia mwaka 1985, hadi 1990, kabla ya kustaafu uongozi. Siku hiyo hiyo zilipatikana habari kwamba chama cha mapinduzi kilikuwa kimeamua kusimamia usambazaji wa habari za ugonjwa wa Mwl Nyerere kwa kumtuma mwanasiasa mkongwe ,kingunge Ngombale mwiru ambaye pia alikuwa waziri wa tawala za mikoa na serikali za mitaa.
Ubalozi wa Tanzania uingereza nao ulikaririwa ukisema kwamba ulikuwa umeanza kutumia ukurasa wake katika Mtandao wa kompyuta wa internet ( website) kwa ajili ya kutoa taarifa za mara kwa mara kuhusu hali ya afya ya Mwl Nyerere.

Septemba 28: watu mbalimbali waliripotiwa kuitikia wito wa Rais Mkapa wa kumwombea Mwl Nyerere aweze kupona .miongoni mwao ni makamu wa Rais Dk omar Ally Juma aliyeongoza sala ya aina hiyo katika msikiti wa Shadhily ,Dar es salaam iliyoandaliwa na Baraza kuu la waislamu Tanzania ( BAKWATA) na kuhudhuriwa na madhehebu yote ya waislamu na watu mbalimbali ,wakiwemo mawaziri ,mabalozi na wananchi ,dua hiyo ilisomwa na sheikh Sharrif Juneid.
Kutoka London kwenyewe ,balozi wa Tanzania uingereza Dr Abdulkadir Sharrif alisema ya kuwa madaktari walisema kwamba dawa alizokuwa anatumia Mwl Nyerere zilikuwa zinaendelea kumpa nafuu polepole.
Alisema madaktari na wauguzi walikuwa wapo katika chumba alimolazwa Mwl Nyerere kwa saa 24, na walikuwa wanashauri Mwl Nyerere asisumbuliwe na watu waliokuwa wakienda kumwona.
Balozi alisema salamu za kumtakia afya njema Mwl Nyerere zilikuwa zikitumwa kutoka kwa viongozi mbalimbali duniani wakiwemo Malkia Elizabeth wa uingereza, Rais Muamar Gaddafi wa Libya ,waziri mkuu wa uingereza Tony Blair na watu binafsi.
Alisema kwamba watanzania Wengi walio nje ,hasa marekani ,Australia, Canada, uingereza, umoja wa falme za kiarabu na Japan nao walikuwa wakituma salamu za kumtakia afya njema Mwl Nyerere
Septemba 28: mwandishi wa Rais Geoffrey Nkurlu alitoa taarifa kutoka Ikulu ,Dar es salaam kwamba Mwl alikuwa akiendelea vizuri na kupata nafuu polepole Nkurlu alithibitisha kuondoka kwa ngombale mwiru kwenda London na kwamba kuanzia wakati huo ofisi ya rais ingekuwa inatoa taarifa kuhusu hali ya Mwl Nyerere kila Siku saa 12 jioni.
Septemba 29: Nkurlu alitoa taarifa kwamba hali ya Mwl Ilikuwa haijabadilika sana na ilikuwa imegundulika kwamba alikuwa anasumbuliwa na homa ya manjano ( jaundice) Nkurlu alisema katika taarifa yake kwamba hata hivyo madaktari wa Mwl walieleza ya kuwa kujitokeza kwa ugonjwa wa manjano ni jambo la kawaida na hivyo hakukuwa na sababu za wasiwasi, kipimo cha damu ( haemoglobin) cha Mwl Nyerere kilikuwa kimepanda na kuwezesha mwili kutoa chembe chembe za damu za kinga ya mwili ,alisema Mwl alikuwa anaweza kujieleza vyema alipokuwa anahitaji kitu na kwamba jana yake alikuwa ametumia muda mrefu akiwa amelala.
Siku hiyo hiyo, Mtoto wa Mwl Nyerere ,makongoro Nyerere alizungumza na waandishi wa habari kwenye ukumbi wa idara ya habari( MAELEZO), Dar es salaam ambako pamoja na mambo mengine ,alisema alikuwa ameshindwa kwenda London kumwona baba yake kwa
Vile hakuwa na fedha.
Septemba 30: katika taarifa yake, Nkurlu alisema kuwa Mwl Nyerere alikuwa ameanza kupata nguvu kidogo baada ya kuanza kulishwa kwa mpira,alisema Mwl alikuwa ameweza kufungua macho mara kwa mara na kujitahidi kugeuka bila msaada ,huku akionyesha dalili za kuelewa mambo yaliyokuwa yakitokea katika mazingira yaliyokuwa yanamzunguka na matatizo madogo ya kupumua yaliyokuwa yameanza kujitokeza yalikuwa yamedhibitiwa.
Nkurlu alisema pia kuwa Abdulwakil aliyelazwa katika hospitali hiyo ya st. Thomas alikuwa ameanza kutibiwa kutokana na matatizo ya moyo na miguu yanayomkabili ,ingawa vyanzo vya habari huru vilisema kwamba uchunguzi wa miguu ya Abdulwakil ulithibitishwa na damu kutozunguka.
Habari nyingine mjini Dar es salaam zilisema kwamba juhudi za kumpeleka London ,kiongozi wa kikundi cha wanamaombi padri felician nkwera kwenda kumuombea Mwl Nyerere zilikuwa zimegonga ukuta baada ya kukataliwa na serikali ,kutokana na kuonekana kwamba ingekuwa inajiingiza kwenye mgogoro kati ya wanamaombi na Kanisa katoliki.
Habari za uhakika zilizopatikana dar es salaam zilisema jitihada za kumpeleka London padri nkwera zilikuwa zikifanywa kwa pamoja na mama maria Nyerere na binti yake Mwl ,Anna.
Oktoba mosi, Nkurlu alitoa taarifa nne zilizoeleza kwamba hali ya Mwl ilikuwa imebadilika ghafla jana yake Usiku na hivyo kusababisha apelekwe katika chumba cha watu mahututi ( intensive care unit) ambako alikuwa akisaidiwa na mashine kupumua.
Nkurlu alitoa taarifa kwanza saa 9.56 asubuhi ambako alisema kwamba " hali ya Mwl Nyerere imebadilika ghafla jana Usiku na madaktari wake wameieleza kwamba sio Nzuri.
Hata hivyo madaktari wanajitahidi kwa kila hali kumhudumia baba wa taifa ambaye hivi sasa hana kauli"
Taarifa ya pili saa 6.58 ambayo pamoja na mambo méngine ,ilieleza kuwa " matokeo ya vipimo vya jaundice ( homa ya manjano) yameonyesha kwamba homa imeongezeka . hata hivyo sasa madaktari wanaomhudumia wanakutana kufanya tathmini nzima ya afya yake.
" Rais Benjamin Mkapa anafuatilia hali ya baba wa taifa kwa karibu sana na anawaomba watanzania waendelee kumwombea Mwl Nyerere.
Saa 9.54 Nkurlu alitoa taarifa nyingine ,taarifa hiyo ilisema " madaktari wanaomtibu Mwl Nyerere wanaendelea kuielezea hali yake kuwa ni mbaya na wanajitahidi kwa kila njia kuokoa maisha yake .
Madaktari wamempatia Mwl Nyerere dawa ili alale na kupumzika hivyo siyo rahisi kutathmini hali halisi iwapo anatambua mazingira yanayomzunguka".
Taarifa ya mwisho ya Nkurlu aliitoa saa 12.59 jioni ambayo ilieleza mambo hayo yaliyokuwamo katika taarifa ya tatu.
Oktoba 3: watoto wengine wa Mwl ,Madaraka na Pauleta waliwasili London kuungana na wenzao Anna na Rosemary na mama yao, mama maria Nyerere, Mtoto mwingine , makongoro ,alitarajiwa kuwasili London kesho yake.
Oktoba 4: madaktari wasema bado hawajakata tamaa kwani uwezekano wa kuokoa maisha ya Mwl ulikuwa bado upo. Daktari wake Profesa David mwakyusa alikaririwa akiiambia BBC kwamba matumaini ya kuokoa maisha ya Mwl yalikuwa bado yapo ,ingawa alikuwa bado ni mahututi.
Madaktari wa Mwl pia walinukuliwa wakisema walikuwa wameweka utaratibu maalum wa kumuona Mwl ICU kwa sababu walikuwapo wagonjwa Wengi katika chumba hicho na kwamba ungekuwapo uwezekano wa kumwambukiza Mwl vijidudu kama watu wengi wangekwenda kwa pamoja kumuona.
Oktoba :5: Rais bill Clinton wa marekani akaririwa akisema ,kupitia kwa balozi wake katika Tanzania ,Charles Stith, kwamba alikuwa tayari kutoa msaada wa matibabu kwa Mwl kwa kuwatuma madaktari kwenda hospitalini alikolazwa kusaidiana na waliokuwa wanamtibu au kwa kumsafirisha hadi marekani ili atibiwe na madaktari bingwa wa huko.
Madaktari wa Mwl pia walifanya majaribio ya kuiondoa mashine iliyokuwa inamsaidia kupumua baada ya kuona kwamba alikuwa na uwezo wa kupumua bila msaada wa mashine, taarifa ya Ikulu nayo ilisema kwamba homa ya manjano ilikuwa imepungua na madaktari wamembadilishia dawa nyingine ya homa ambayo ilikuwa imeonyesha mafanikio.
Oktoba 6: Taarifa ya Ikulu iliwakariri madaktari wake wakisema kwamba hali ya Mwl ilikuwa inaonyesha kwamba viungo kadhaa vya Mwl vilivyokuwa na matatizo vilikuwa vimepata nafuu, na hakukuwapo na magonjwa ya ziada ambayo yalikuwa yamejitokeza.
Taarifa ya Ikulu pia ilizishukuru uingereza na Marekani kwa kueleza nia yao ya kusaidia katika matibabu ya Mwl.
Makamu mwenyekiti mstaafu wa CCM Mzee Rashid Kawawa na jenerali mstaafu wa jeshi la wananchi wa Tanzania ,David musuguri wawasili London ili kumwona Mwl.
Oktoba 7: hali ya Mwl yaripotiwa kutia matumaini ya kupata nafuu na kwamba jana yake aliweza kufumbua macho mara kwa mara, ingawa madaktari wake kwa mujibu wa taarifa ya Ikulu ,walikuwa wameamua aendelee kutumia mashine ya kumsaidia kupumua kwa wiki moja zaidi pamoja na Sawa za usingizi.
Anna mke wa Rais Mkapa ambaye alikuwa London akisaidiana na mama maria Nyerere kumuuguza Mwl arejea Dar es salaam.
Kawawa na Jenerali musuguri wamwona Mwl na kumjulia hali.
Oktoba : 8 Taarifa ya Ikulu yaeleza kwamba Mwl alikuwa anaendelea kupata nafuu polepole na kwamba kuendelea kutumia ya kumsaidia kupumua ,kulikuwa kumemwezesha Mwl kuwa na nguvu za ziada.
Taarifa iliyotolewa baadae na Ikulu ilisema hali ya Mwl ilikuwa imebadilika ghafla na kuwa mbaya na hivyo ikalazimika ahamishiwe katika chumba cha wagonjwa mahtuti(ICU).
Oktoba 9: na 10: hali ya Mwl ilikuwa bado mbaya na habari zilizotolewa na Ikulu zilisema madaktari walikuwa wamefanikiwa kudhibiti hali yake isiendelee kudhoofu zaidi na kuacha kumpa dawa za usingizi Kama ambavyo walikuwa wakifanya awali.
Oktoba 11: madaktari waliokuwa wakimtibu Mwl walisema hali yake ilikuwa bado siyo Nzuri na hivyo walikuwa wameamua kumfanyia uchunguzi wa ubongo.
Oktoba 12: Mwl alikuwa hajazinduka kwa saa 100, tangu madaktari walipokuwa wameacha kumpatia dawa za usingizi,baada ya hali yake kubadilika ghafla.
Taarifa zilizopatikana baadae kutoka London zilisema madaktari baada ya kuchunguza ubongo wa Mwl waligundua kuwa ubongo wake ulikuwa na matatizo na asingeweza kuamka tena.
Oktoba "13: Balozi wa Tanzania nchini uingereza Abdulkdir Sharrif athibitisha kuwa matokeo ya uchunguzi wa madaktari kuhusu ubongo wa Mwl Nyerere hayakuwa ya kutia matumaini.
" Ni ya kuondoa matumaini .....viungo vyake vyote muhimu havionyeshi kupata nafuu....matumaini yaliyopo siyo makubwa," alisema balozi alipohojiwa na shirika la utangazaji la uingereza ( BBC).
Oktoba 14: Mtoto wa Mwl Nyerere ,makongoro alikaririwa akisema kwamba familia yao ilikuwa inasubiri msiba kwa kuwa ilikuwa ni dhahiri kwamba ilikuwa haiwezi kurejea naye nyumbani akiwa hai.
"Tupo katika hali ya uchungu mkubwa sana kwa kuwa ndiyo mara ya kwanza tunafiwa na mzazi, lakini hatuna la kufanya kwa sababu hiyo ni kazi ya mungu na hakuna mtu anayeweza kuishi milele," Makongoro alikaririwa akisema alipohojiwa na BBC.
Oktoba 14: saa sita kasoro dakika tano mchana Rais Benjamin Mkapa alitangazia taifa kutokea kifo cha Mwl Nyerere. Akitangaza kupitia Redio Tanzania Dar es salaam (RTD) na Televisheni ya ITV, Rais Mkapa alisema Mwl alifariki dunia saa 4:30 saa za afrika mashariki katika hospitali ya St. Thomas, London, uingereza alikokuwa amelazwa.
Kwa muda mrefu Mwl amekuwa mwanasiasa maarufu wa Afrika na hata duniani ,na hasa amekuwa nguzo na ngao kubwa ya mwelekeo na utulivu wa kisiasa wa Tanzania kiasi cha kuitwa baba wa taifa.
Aliongoza mapambano ya Uhuru wa Tanganyika ,ikiwa ni pamoja na kuanzishwa kwa chama cha TANU mwaka 1954 akawa waziri mkuu wakati wa Uhuru mwaka 1961, Rais wa Tanganyika mwaka 1962, na Rais wa Tanzania kuanzia mwaka 1964, Mwl Nyerere aliiongoza Tanganyika na Tanzania kwa miaka 24, kabla ya kukabidhi madaraka kwa Ali Hassan Mwingi mwaka 1985.
Mungu iweke roho ya Mwl Nyerere mahali pema peponi .
