Ndoa za kidijitali
Ndoa ya sasa imejaa usasa, na usasa wenyewe hauchangii kuleta uchanya wowote Bali kuendelea kuisambaratisha ndoa ya karne hii. Nini hasaa kimechangia hali hii katika jamii zetu? Kipindi hiki utaskia kijana ameoa na baada ya mwaka mmoja amempa mkewe talaka. Jibu sahihi la swali hili ni kwamba uchumba na kipindi cha kuchumbiana kimekosa umuhimu katika maisha ya sasa. Vijana wengi hutumia kipindi hiki kujistarehesha na Si kuelewana kitabia ilivyokuwa awali. Vijana hawajui kwamba uchumba ulioachika ni bora kuliko ndoa iliyokosa amani na furaha.
Ndoa za awali zilijengwa na wazazi waliojaa busara na hekima. Wazazi hawa walithibiti wana wao na kuwakanya sawasawa kuhusiana na makali yaliyo katika ndoa, sembuse wazazi wa sasa wanaowaacha wana wao kujiamulia hatima ya maisha yao. Kipindi cha wazazi wetu, urembo na umbo la kutazamwa havikuwa vigezo vya kutathmini uzuri wa mke, Bali heshima na bidii katika kazi viliangaliwa hivyo kupelekea kila mwanamke kujikaza na kutia bidii kazini. Lakini karne hii mambo ni kinyume, kiukweli tumeziacha mila zetu na sasa twaila miande ya utumwa wa usasa katika ndoa.
Wengi wa vijana wa sasa hasaa jinsia ya kiume, utawaona wanazingatia kigezo cha sura na maumbo ya kujishebedua katika uteuzi wa wachumba uzuri wa ndani yaani tabia. Suala hili limewafanya wale wa jinsia ya kike kujitia kwenye utumwa wa kuboresha maumbo yao ili kujinadi sawasawa. Na vipi kuhusu urembo? Hao hao wameanza kuzijichubua ngozi zao ili kuwavutia watakao waona.
Ndoa imezama bila kuibuka kwa sababu suala la usawa limeikwaza mno. Imekuwa vita baina ya wachumba, je, nani anafaa kusema katika ndoa. Utamwona mwanamke anataka nafasi sawa na mwanamume katika ndoa. Kimsingi ni kwamba hata kwenye maandiko Matakatifu usawa huo haujaangaziwa. Yaani tuseme usawa huu umeletwa na jinamizi hili la usasa. Hata hivyo tunapokimbilia usawa huu tukumbuke kwamba kila mmoja ana jukumu ambalo anafaa kutekeleza, ndo kwa maana mume habebi mimba.
Kutonesha kidonda zaidi ni kwamba mataifa mengi duniani yamehalalisha haramu katika ndoa. Kama vile,ndoa baina ya watu wa jinsia moja. Hata kukubali kufunga ndoa hizo mbele ya halaiki ya watu!
Kiukweli usasa umeinajisi ndoa maradufu. Tusipoziba ufa huu basi tutalazimika kujenga ukuta upya kwa ajili ya kizazi kijacho.
na;
Francis Onyinkwa
Mwanafunzi-Chuo Kikuu Cha Kenyatta
